




**************
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imetoa msaada wa mifuko ya saruji kwa kituo cha watoto yatima cha Mama wa Huruma, kilichopo eneo la Madale Wazo Hill nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mifuko hiyo 70 ya saruji imekabidhiwa juzi katika kituo hicho na Kaimu Mkuu wa Biashara TTCL Kanda ya Dar es Salaam, Bw. David Dirisha kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo.
Akikabidhi msaada huo, Bw. Dirisha alisema kampuni imetoa msaada huo ili kusaidia ujenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima na wale wenye mahitaji maalum. Alisema msaada huo waliokabidhi utasaidia kituo hicho kuwa na majengo yake yenyewe kwani kwa sasa wamejihifadhi katika eneo dogo na ambalo sio rafiki sana kwa watoto. Kwa upande wake, Mtawa anayewalea watoto hao, Sr. Christina akipokea msaada huo alisema, anaishukuru kampuni ya TTCL kwa msaada huo; kwani umekuwa chachu ya kuamini kuwa na wao watakuwa na majengo yao na wataweza kusaidia watoto wengi zaidi.
Aidha ametoa wito kwa wadau wengine watakao guswa zikiwemo kampuni na taasisi mbalimbali kusaidia kituo hicho ili kiweze kukamilisha kwa wakati ujenzi wa majengo yake na hatimaye kuhudumia watoto wengi zaidi huku kukiwa na usalama wa kutosha. Hii ni mara ya pili kwa TTCL kukichangia kituo hicho mifuko ya saruji kwani mwaka jana pia ilitoa msaada wa saruji kwa kituo hicho cha watoto yatima cha Mama wa Huruma ambacho kwa sasa kina idadi ya watoto 56 ambapo wavulana ni 26 na wasichana 30.